Maktaba ya Uongozi jijini Dar es Salaam Kuzinduliwa Leo

27 Oktoba, 2022: Maktaba yetu ya Uongozi iliyopo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, itazinduliwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Mb). 

Aidha, tukio hilo litajumuisha utambulisho wa toleo la Kiswahili la tawasifu ya Rais wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, “Maisha Yangu, Kusudi Langu: Kumbukizi ya Rais wa Tanzania”. Hapo awali, kitabu hiki kiliandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kuzinduliwa Novemba, 2019 na hayati John Pombe Magufuli, Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati wa uzinduzi, Mheshimiwa Rais aliiagiza Taasisi ya UONGOZI itafsiri kitabu hicho kwenda kwenye lugha ya Kiswahili ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Washiriki kwenye tukio hili ni pamoja na mke wa Rais Mstaafu Mkapa, Mama Anna Mkapa; Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI; viongozi waandamizi kutoka kwenye sekta za umma na binafsi; washirika wa maendeleo; na wanachama wa Maktaba hiyo. 

Maktaba ya Uongozi ilianzishwa mnamo mwaka 2012 kwa lengo la kuhamasisha utamaduni wa kutoa maarifa na kujisomea nchini na Barani Afrika kwa ujumla. Kupitia Maktaba hii, viongozi, watafiti, wanafunzi na jamii kwa ujumla, wanaweza kufikia machapisho ya masuala ya uongozi na maendeleo endelevu yanayoendana na mabadiliko mbalimbali duniani. Maktaba ina vitabu na majarida zaidi ya 50,000, ikiwemo vile vilivyochapishwa na katika mifumo ya kielektroniki. 

Ushiriki wa ana kwa ana katika tukio hili ni kwa mwaliko pekee. Aidha, tukio hili litaruka mubashara kupitia akaunti yetu ya YouTube.  

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s